Tuesday, October 29, 2013

KINANA AZIMA MAPINDUZI



Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alilazimika kuzima mapinduzi yaliyokuwa yamepangwa kuwang’oa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana ya chama hicho (UVCCM), Sadifa Juma Khamis na makamu wake, Mboni Muhita.

Jana Kinana akifungua mkutano wa Baraza Kuu la jumuiya hiyo, aliweka bayana kuwa mkutano huo haukuwa kwa ajili ya “kuibomoa UVCCM, bali kuijenga”, kauli ambayo inatajwa kuwa iliwavunja nguvu wajumbe waliokuwa wamepanga kuanzisha harakati za kuwatoa madarakani viongozi hao.

Habari zaidi kutoka Dodoma zilisema kauli ya Kinana iliongeza nguvu harakati za kujinasua za Sadifa ambaye usiku wa kuamkia jana, alikesha akifanya vikao vya kuwaomba radhi wenyeviti wa UVCCM wa mikoa na baadaye wajumbe wote wa Baraza Kuu.

“Hatua hiyo nadhani imemsaidia sana maana wenzake ndani ya umoja huo hawaridhiki na jinsi mambo yanavyokwenda, pamoja na uongozi wake. Wanaona kama hakidhi standards (viwango) zao,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya mkutano huo.

Hii ni mara ya pili kwa Katibu Mkuu huyo kumwokoa Sadifa, kwani Septemba mwaka huu, alilazimika kuingilia kati mgogoro ambao uliibuka katika kikao cha Baraza Kuu la jumuiya hiyo Visiwani Zanzibar baada ya wajumbe kutaka kumwajibisha kwa madai kwamba alikiuka kanuni za uteuzi wa wakuu wa idara za UVCCM.


Pamoja na kauli elekezi ya Kinana, Sadifa ambaye pia ni Mbunge wa Donge, Zanzibar alilazimika kucheza sarakasi zilizomwezesha kuzima mapinduzi yaliyokuwa yameandaliwa dhidi yake. Mwenyekiti huyo aliongoza kikao cha Baraza Kuu kwa saa tatu na kukamilisha ajenda zilizokuwa zimepangwa, ikiwa ni pamoja na kuwaidhinisha wakuu wapya wa idara za jumuiya hiyo, kisha aliahirisha mkutano huo mara tu baada ya kuibuliwa kwa hoja ya kutaka kumjadili.


Habari zilizolifikia gazeti hili jana jioni zilisema, Mwenyekiti wa UVCCM, Mkoa wa Mbeya, Amani Kajuna ndiye aliyeibua hoja ya kutaka Sadifa ajadiliwe kutokana na kile alichosema kuwa kiongozi huyo ameifanya jumuiya hiyo kushindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo.


“Kama tunataka kusonga mbele katika jumuiya yetu, lazima tuhakikishe kwamba tunaisafisha nyumba yetu ili tukitoka hapa wote tuwe tunazungumza lugha moja. Kwa hiyo napendekeza mwenyekiti atoke nje ili tumjadili,” chanzo chetu kilimnukuu Kajuna.


Habari zaidi zilidai mapendekezo hayo ni kama yaliungwa mkono na baadhi ya wajumbe, akiwamo Mwenyekiti wa UVCCM wa Mkoa wa Dodoma, Henry Msunga ambaye alisimama na kusema: “Hiyo ni hoja ya msingi sana”.


Hata hivyo, wakati wajumbe wengine wengi wakiwa wameinua mikono yao juu wakitaka kuchangia pendekezo hilo, Sadifa alisimama na kuanza kuzungumza huku akiomba msamaha kwa upungufu wa kiuongozi unaojitokeza na katika hali isiyotarajiwa aliahirisha rasmi mkutano huo.









Kajuna na Msunga kwa nyakati tofauti jana, walilithibitishia gazeti hili kuwapo kwa matukio hayo, lakini walikataa kuyazungumzia kwa undani huku wakisema kuwa bado wana fursa katika vikao vijavyo kwa ajili ya kurekebisha mambo ndani ya jumuiya hiyo.

No comments:

Post a Comment