Tuesday, November 12, 2013

MKUU WA SHULE ABAMBWA AKIVUJISHA MAJIBU YA MTIHANI

MKUU wa Shule ya Sekondari ya Nkinto wilaya ya Mkalama, Monica Sebastian (30) na mwalimu wa kawaida wa shule hiyo, Agaloslo Otieno (32), wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma ya kuvujisha matihani wa kidato cha nne unaoendelea kufanyika hivi sasa nchini kote.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Geofrey Kamwela, alisema tukio hilo lilitokea juzi, saa tatu usiku, katika shule hiyo kata ya Mwangeza tarafa ya Kirumi wilayani humo.

Alisema kuwa Mwalimu Agaloslo akiwa anasimamia mtihani katika Shule ya Sekondari Mwangeza, alikuwa anaandika baadhi ya maswali ya Kiswahili na Civics kwenye simu yake ya kingajani na kumtumia Mwalimu Monica, akiwa shuleni kwake Nkinto.

Kamwela alisema baada ya Monica kupata maswali hayo, alikuwa anayatafutia majibu akiwa chooni na wanafunzi walikuwa wanamfuata huko huko chooni ili awapatie majibu hayo.

"Lengo lao ilikuwa ni kuwasaidia wanafunzi ili waweze kufanya vizuri katika mtihani wao wa kidato cha nne mwaka huu. Wanafunzi waliambiwa kuwa wawe wanadanganya kwamba wanaenda kujisadia chooni ili wakapatiwe majibu na mkuu wa shule," alisema kamanda huyo na kuongeza; "Uchunguzi wa awali wa polisi unaonyesha kuwa, uvunjishaji huo ulifanyika kwa nyakati tofauti kati ya Mkuu wa Shule Monica na Mwalimu Agaloslo akiwa anasimamia mtihani huo katika shule nyingine.
“Baada ya Mwalimu Monica kutumiwa maswali alikuwa anajificha chooni na wanafunzi kwa nyakati tofauti huomba ruhusa kwa wasimamizi kwenda chooni kwa nia ya kujisaidia, ambapo humkuta mwalimu huyo na kuwapa maelekezo ya namna ya kujibu maswali hayo," alisema.

Alisema baada ya polisi kupata taarifa ya siri kutoka kwa wasamaria wema, waliweka mtego shuleni Nkinto na kufanikiwa kumkamata Mwalimu Monica, huku simu yake ikiwa na baadhi ya maswali ya mtihani.

Alisema polisi inaendelea na upelelezi zaidi, na kwamba mara utakapomalizika, watuhumiwa watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma inayowakabili.

No comments:

Post a Comment